Wababe
wa Morogoro, Mtibwa Sugar, hawana hofu hata kidogo. Wanasema wapinzani
wao Simba wasifikirie kutwaa pointi tatu kutoka kwao kwa kuwa wanaijua
vyema safu yao ya ushambuliaji ambayo ni zao lao, akiwemo Shiza Kichuya,
Mohamed Ibrahimu ‘Mo’, Mzamiru Yassin na Juma Luizio, kwa kuwa ni
wachezaji waliowalea wenyewe na wanatambua upungufu wao.
Simba
na Mtibwa zinatarajiwa kukutana keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa
Jamhuri, Morogoro, baada ya ligi kusimama kwa muda kupisha michuano ya
Kombe la Mapinduzi iliyomalizika Ijumaa iliyopita huku Azam ikitwaa
ubingwa huo.
Akizungumza na Championi Jumatatu,
Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema wanaiheshimu
Simba kwa kuwa ni timu inayoongoza msimamo wa ligi na ipo vizuri lakini
wasitegemee kuwafunga katika uwanja wao wa nyumbani, kwa kuwa wanaijua
vilivyo safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kutokana na asilimia kubwa ya
wachezaji wao wote, wametokea Mtibwa, hivyo wanazifahamu mbinu zao.
“Tuko
vizuri kukabiliana na Simba kuelekea mchezo wetu wa Jumatano kwani
kipindi hiki cha mapumziko mafupi ya wiki mbili, kimetusaidia, tumefanya
mazoezi makali ambayo yametusaidia kukiimarisha kikosi.
“Lengo
letu ni kuhakikisha hatufungwi katika mechi zetu zilizobakia katika
mzunguko wa pili kwani kuna ushindani mkubwa kwa kuwa kila timu
inahitaji kushinda na sisi hatujapoteza mchezo wetu hata mmoja, hivyo
Simba wasitarajie kupata pointi tatu hapa kwetu.
“Hatuihofii
safu ya ushambuliaji ya Simba kwani tunaifahamu vyema safu yote ya
ushambuliaji kwa kuwa wote wametoka Mtibwa Sugar na tumewalea wenyewe na
tunatambua vizuri mbinu zao, hivyo hazitupi shida.
“Wachezaji
wetu wana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo, japokuwa
tunaiheshimu Simba kwa kuwa inaongoza msimamo, tunahitaji kushinda
katika uwanja wetu wa nyumbani kwa kushirikiana na mashabiki wetu ambao
watatupa sapoti kubwa,” alisema Kifaru.
Mtibwa
itaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo baada ya
kukusanya pointi 30, wakati Simba ipo kileleni na pointi 44.
0 Maoni:
Post a Comment