Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemwondoa Mwamuzi Hussein Athuman kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha Ligi hiyo.
Mwamuzi Hussein Athuman kutoka Mkoa wa Katavi alichezesha mchezo namba 150 uliozikutanisha timu za Majimaji ya Songea na Young Africans ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Kadhalika
Young Africans imepigwa faini ya jumla ya Sh. 1,000,000 (milioni moja)
kutokana na timu yao kutoingia vyumbani, na pia kutumia mlango usio
rasmi wakati wa kuingia uwanjani, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni
ya 14 (13) na (14) ya Ligi Kuu. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia
Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
Mwamuzi Ngole Mwangole:
Mwamuzi huyo wa kati, Ngole Mwangole wa Mbeya amepewa barua ya onyo
kali na kumtaka aongeze umakini wakati akichezesha mechi za Ligi Kuu ya
Vodacom baada ya kubainika kukataa bao lililoonekana kutokuwa na
mushkeli la Mtibwa Sugar dhidi ya JKT Ruvu katika mechi iliyofanyika
Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Licha
ya kujitetea, lakini kamati haikuridhika na maelezo yake. Hata hivyo,
kwa kuzingatia kuwa Bw. Mwangole alikuwa Mwamuzi Bora wa msimu uliopita
(2015/2016) na hiyo ndiyo mara yake ya kwanza kuonekana kufanya uamuzi
uliokosa umakini wakati akichezesha, TFF imeamua kumpa onyo.
Mechi
namba 141 (Mwadui FC vs Kagera Sugar). Beki wa Kagera Sugar, Godfrey
Taita anapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi baada ya
mechi na kuwatolea lugha chafu na vitisho kabla ya benchi la ufundi la
timu yake pamoja na askari polisi kuingilia kati na kudhibiti kadhia
hiyo.
Mechi
namba 151 (Mtibwa Sugar vs Simba). Baada ya mchezo kumalizika mashabiki
waliingia uwanjani kwa wingi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa
wachezaji, waamuzi na waandishi wa habari. Pia kamera ya Azam Tv upande
wa goli la Kusini iliangushwa na washabiki hao.
Vilevile
sehemu ya kuchezea (pitch) ya Uwanja wa Jamhuri iko katika hali mbaya
ambapo inahitaji marekebisho makubwa ili iweze kuendelea kutumika kwa
ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.
TFF
imebaini kuwa kitendo cha washabiki kuingia uwanjani baada ya filimbi
ya mwisho, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni lakini pia kilichangiwa
na askari polisi kutokuwa makini katika majukumu yao ya kusimamia
usalama uwanjani na badala yake kuelekeza umakini katika kutazama mechi.
Hivyo,
Uwanja umesimamishwa kutumika kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom
ili kutoa fursa kwa wamiliki kufanya marekebisho makubwa kwenye eneo la
kuchezea (pitch), na pia askari polisi kupata maelekezo ya kutosha ya
jinsi ya kusimamia usalama uwanjani badala ya kutazama mechi. Kama
marekebisho hayatafanyika, uwanja huo hautatumika kwa ajili ya mechi za
Ligi Kuu ya Vodacom.
LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi
namba 34 (Pamba vs Friends Rangers). Kamishna wa mechi hiyo Mnenge
Suluja amepewa Onyo Kali kwa kutoripoti kitendo cha timu ya Pamba
kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa na
wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni
ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi
namba 35 (Kiluvya United vs Lipuli). Timu ya Lipuli imepewa Onyo Kali
kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) ikiwa
na wawakilishi watatu badala ya wanne. Kitendo hicho ni kinyume na
Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia
mshabiki wa Kiluvya United, Bw. Athuman Mzongela anapelekwa Kamati ya
Nidhamu kwa kuwavamia waamuzi na kutaka kuwapiga wakati wa mapumziko.
Hata baada ya mchezo aliendelea kuwatolea lugha chafu waamuzi na
Msimamizi wa Kituo.
Mechi
namba 36 (African Sports vs Ashanti United). Daktari wa Ashanti United,
Andrea Mbuguni amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh. 200,000
kwa kuondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea lugha chafu Mwamuzi
Msaidizi namba moja.
Mechi
namba 38 (Lipuli vs Mshikamano FC). Kocha wa Mshikamano FC, Hamisi
Kinonda amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya
kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga muda wa nyongeza wa dakika tano, na
kumtolea lugha ya matusi Mwamuzi wa Akiba. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa
Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Wachezaji
wa Mshikamano FC, John Mbise jezi namba 9, Abdallah Makuburi (5), Ally
Mangosongo (12) na kipa Steven Peter (1) wanapelekwa Kamati ya Nidhamu
ya TFF kwa kumshambulia Mwamuzi Bryson A. Msuya.
Lakini
pia Mwamuzi Bryson A. Msuya amefungiwa mwaka mmoja kwa kutozingatia
sheria ipasavyo wakati akitoa penalti dhidi ya timu ya Mshikamano FC, na
ripoti yake kufanana na ile ya Kamishna.
Mwamuzi
Msaidizi Namba Moja, Makongo Katuma amefutwa katika orodha ya waamuzi
wanaotambuliwa na TFF kwa kuwapiga vichwa wachezaji wawili wa Mshikamano
FC wakati Mwamuzi wa Kati alipokuwa akishambuliwa na wachezaji wa timu
hiyo wakati wakipinga adhabu ya penalti dhidi yao.
Adhabu
hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) na 38(1c) na (1e) za Ligi Daraja
la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Mwamuzi Katuma pia alipata alama
za chini ambazo zisingemruhusu kuendelea kuchezesha Ligi Daraja la
Kwanza.
Naye
Mwamuzi wa Akiba, Hashim Mgimba ameondolewa kwenye ratiba kwa kuonyesha
muda wa nyongeza (added time) tofauti na ule alioelekezwa na Mwamuzi.
Adhabu dhidi ya Mgimba imezingatia Kanuni ya 38(1d) ya Ligi Daraja la
Kwanza.
Kamishna
wa mechi hiyo Fidelis Ndenga wa Njombe ameondolewa kwenye ratiba ya
makamishna kwa taarifa yake kufanana na ile ya Mwamuzi. Adhabu hiyo
imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu
Udhibiti wa Makamishna.
Pia
Kamati imetoa mwito kwa vyombo vya usalama (askari polisi) kutumia
nguvu za wastani katika kutuliza ghasia viwanjani, hasa pale wanapotaka
kushughulikia eneo linalohusu wachezaji.
Uwanja
wa Kichangani umeondolewa kutumika kwa mechi za Ligi, hivyo klabu za
Iringa sasa timu zao zitatumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini humo
kwa mechi zao la Ligi. Uwanja huo ulikuwa kwenye matengenezo ambayo
tayari yamekamilika.
Mechi
namba 39 (Polisi Dar vs Pamba FC). Klabu ya Pamba imepewa Onyo Kali kwa
kutofika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting).
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi
namba 33 (KMC vs JKT Mlale). Kocha wa JKT Mlale, Edgar Msabila
amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 baada ya
kuondolewa kwenye benchi la ufundi (orderd off) kwa kutoa lugha chafu.
Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi
namba 38 (Kimondo FC vs Njombe Mji). Kocha wa Njombe Mji, Abdul Banyai
amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kumtolea
Mwamuzi lugha ya matusi, na kulazimisha wachezaji wake wajiangushe ili
kupoteza muda.
Mechi
namba 40 (Coastal Union vs Kurugenzi). Wachezaji wawili wa Kurugenzi;
Kipa Hamza Mpatula na Optatus Lupekenya wamefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kosa la kupigana wakiwa
uwanjani baada ya mechi kumalizika. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni
ya 37(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Wachezaji.
Mechi
namba 36 (Rhino Rangers vs Polisi Mara). Klabu ya Rhino Rangers
imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika
20. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Mechi
namba 38 (Mgambo Shooting vs Rhino Rangers FC). Kocha wa Mgambo, Moka
Shabani amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa kutoa
lugha ya matusi kwa Mwamuzi wakati timu zikielekea vyumbani baada ya
kumalizika kipindi cha kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya
40(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
LIGI DARAJA LA PILI
Mechi
namba 17 (Abajalo vs Burkina Faso). Klabu ya Burkina Faso imepigwa
faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre
match meeting). Adhabu imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la
Pili kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi
namba 18 (Cosmopolitan vs Changanyikeni). Klabu ya Changanyikeni FC
imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuingia
uwanjani kushangilia ushindi baada ya filimbi ya mwisho. Adhabu hiyo ni
kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Udhibiti wa
Klabu.
Mechi
namba 19 (Kariakoo vs Cosmopolitan). Klabu ya Kariakoo imepewa Onyo
Kali kwa timu yake kutokuwa na daktari katika mechi hiyo. Adhabu hiyo
imezingatia Kanuni ya 14(3).
Mechi
namba 16 (Sabasaba vs Namungo). Klabu ya Sabasaba imepewa Onyo Kali
kutokana na washabiki wake kuwazonga waamuzi wakati wakielekea vyumbani
baada ya mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro
kumalizika. Uamuzi huo umezingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la
Pili.
Mechi
namba 17 (Mawezi Market vs Mkamba Rangers). Mkamba Rangers imepigwa
faini ya sh. 100,000 kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mechi (pre
match meeting), na pia kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 35. Adhabu
hiyo imezingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili.
Mechi
namba 19 (Namungo vs Mighty Elephant). Mighty Elephant imepigwa faini
ya sh. 100,000 kutokana na wachezaji wa akiba na viongozi wake kuingia
uwanjani kushangilia bao la timu yao. Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni
ya 14(7), na adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(47) ya Ligi
Daraja la Pili.
Malalamiko mbalimbali
Malalamiko
ya klabu za Mwadui FC na Polisi Morogoro kuhusu uhalali wa usajili wa
mchezaji wa Stand United, Kheri Mohamed Khalifa na wachezaji wawili wa
Njombe Mji kucheza mechi bila leseni yamepelekwa Kamati ya Sheria na
Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Pia
maombi ya klabu ya Singida United kuhusu kubadilishiwa Mwamuzi kwenye
mechi yao yamepelekwa Kamati ya Waamuzi, wakati maombi ya Alliance
Schools, Friends Rangers FC, The Mighty Elephant na Kariakoo FC
yanayohusu uendeshaji yanashughulikiwa na Sekretarieti ya TPLB.
Kuhusu JKT Ruvu
Katika
mengineyo, Kamati ilipitia maombi ya timu ya JKT Ruvu Stars FC
kubadilisha uwanja wake wa nyumbani kutoka Mabatini mkoani Pwani hadi
Mkwakwani mkoani Tanga kutokana na wachezaji wake 12 wa kikosi cha
kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi mkoani Tanga.
Ombi
hilo limekubaliwa. Kwa mujibu wa Kanuni ya 6(6) ya Ligi Kuu, TFF/TPLB
zina mamlaka ya mwisho kuhamisha kituo cha mchezo kwa sababu inazoona
zinafaa na kwa wakati husika.
Kuhusu Mchezaji Venance Ludovic
Pia
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajiwa kukaa wiki
ijayo kusikiliza malalamiko dhidi ya usajili wa wachezaji mbalimbali
akiwemo mchezaji Venance Joseph Ludovic.
MECHI ZA LEO AZAM SPORTS FEDERATION CUP
Mechi
za raundi ya tano ya mechi za Kombe la Shirikisho la Azam 2016/17 (Azam
Sports Federation Cup - ASFC), zitaendelea tena leo Jamatano Januari 25,
2017 kwa timu za Singida United na Kagera Sugar kucheza kwenye Uwanja wa
Namfua mjini Singida.
Mchezo
mwingine utakaozikutanisha timu za The Mighty Elephant ya Songea na
Mashujaa ya Kigoma katika mchezo utakaofanyika Uwanja Majimaji mjini
Songea.
RATIBA MECHI ZA LEO ZA LIGI YA WANAWAKE
Ligi
ya wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inatarajiwa
kuendelea kesho Jumatano Januari 25, mwaka huu kwa michezo sita – mitatu
kwa kila kundi.
Kundi
A, linatarajiwa kuna na mchezo kati ya JKT Queens Dar es Salaam na
Mburahati Queens pia ya jijini utakaofanyika kwenye Uwanja wa Karume,
Ilala.
0 Maoni:
Post a Comment