Mara Nyingi mechi ya Simba na Yanga huacha matukio ya kukumbukwa
kwenye soka la bongo kutokana na ukubwa wa mechi husika unaosababishwa
na historia ya timu hizi mbili kongwe kwenye anga la michezo la Tanzania
zilizoanzishwa kabla hata ya uhuru wa Tanganyika.
Kwenye mchezo wa Yanga vs Simba uliochezwa October 1, 2016 na
kumalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1, kuna mambo mengi sana
yalijiri kwenye mechi ile ambayo yameacha alama itakayodumu siku zote.
https://www.kiungomshambuliaji.blogspot.com inakuletea matukio matano (5) yaliyotikisa ndani
ya dakika 90 kutoka kwenye mechi ya Yanga vs Simba iliyopita.
1. GOLI LA AMIS TAMBWE.
Ni goli ambalo lilizua sintofahamu uwanjani na kupelekea mchezo
kusimama kwa dakika kadhaa wakati wachezaji wa Simba wakimzonga mwamuzi
kuhoji uhalali wa goli hilo ambapo walikuwa wanadai Tambwe aliushika
mpira kabla ya kufunga.
Tambwe alifunga goli hilo akipokea pasi ndefu iliyopigwa kutoka
katikati ya uwanja, wakati anaumiliki mpira, uligusa mkono wake kabla ya
kumpita beki wa Simba Novalty Lufunga kisha mrundi huyo kumchambua
golikipa wa Simba wakati huo Vicent Ang’ban na kuweka gozi nyavuni.
2. VURUGU ZA MASHABIKI.
Baada ya Tambwe kufunga goli kwa upande wa Yanga, ambalo mashabiki wa
Simba walitafsiri halikuwa goli halali, wakaanza kufanya vurugu
wakipinga uamuzi wa mwamuzi Martin Saanya kulikubali goli hilo.
Mashabiki wa Simba walianza kung’oa viti na kuvitupa chini, ilibidi
polisi kutumia mabomu ya machozi kudhibiti vurugu hizo ambazo awali
zilianzia nje ya uwanja ambapo mashabiki wa timu zote walivunja mageti
wakati wa kuingia uwanjani kwa sababu ya wingi wao huku mashine za
kieletroniki zikishindwa kwenda na kasi ya wingi wa watu
3. KADI NYEKUNDU YA JONAS MKUDE.
Mwamuzi wa mchezo huo Martin Saanya alimtoa nje kwa kadi nyekundu
nahodha wa Simba Jonas Mkude lakini haikueleweka mara moja sababu
ilikuwa ni nini kwa sababu Mkude alionekana kubishana kwa ukali kwa muda
mrefu na mwamuzi pengine ikadhaniwa huenda alimtolea lugha chafu.
Lakini katika mabishano kati ya Mkude na Saanya (mwamuzi) pamoja na
baadhi ya wachezaji wa Simba, mwamuzi alionekana kuyumba na kuanguka
chini kitendo kilichotafsiriwa huenda Mkude alihusika kwa namna moja au
nyingine kwa mwamuzi huyo kuanguka.
Lakini baadae kamati ya saa 72 ilipitia malalamiko ya Simba kuhusu
kadi nyekundu ya Mkude na baadhi ya makosa yaliyofanywa na mwamuzi
Martin Saanya ambapo Mkude alifutiwa kadi nyekundu na Martin Saanya
kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wanaochezesha mechi za ligi kuu
Tanzania bara.
4. KUKATALIWA KWA GOLI LA AJIBU.
Ni miongoni mwa vitu vilivyozua mijadala mikubwa baada ya mchezo wa
Simba na Yanga kumalizika, goli lililofungwa na Ajibu na kukataliwa
lilionekana lilikuwa halali kwa mujibu wa picha za marudio za Azam TV.
Kutokana na uhalali wa goli hilo, mwamuzi wa pembeni siku hiyo (line
one) Samwel Mpenzu pia aliadhibiwa kwa kufungiwa kuchezesha mechi za
ligi kuu Tanzania bara.
5. GOLI LA KUSAWAZISHA LA SHIZA KICHUYA.
Kichuya aliisawazishia Simba dakika za lala salama wakati Yanga
wakiamini watatoka na ushindi wa goli 1-0 siku hiyo.
Kichuya alipiga
kona kutoka Kaskazini Mashariki ya uwanja wa taifa na mpira kwenda moja
kwa moja kwenye nyavu za Ali Mustafa ‘Barthez’ na kuiandikia Simba bao
la kusawazisha.
Goli hilo lilimpa umaarufu mara dufu Kichuya na kuwafanya mashabiki
wa Simba kumuona Kichuya ni mwokozi wao kutokana na bao lake ambalo
liliwafanya Simba kukwepa kipigo cha tatu mfululizo kwenye mechi za
ligi.
Je, nini kitajiri kwenye mechi ya Simba vs Yanga LEO February 25, 2017?
Endelea kuwa karibu na https://www.kiungomshambuliaji.blogspot.com kujua matukio yatakayobamba
ndani na nje ya uwanja.
0 Maoni:
Post a Comment