JANUARI 31, 2015, kiungo kinda raia wa Nigeria, Onyinye Wilfred Ndidi,
alianza kuichezea KRC Genk ya Ubelgiji ambayo alijiunga nayo akitokea
katika moja ya akademi ya Nath Boys ya kwao nchini Nigeria.
Desemba 3, 2016,
alijiunga na mabingwa watetezi wa England, Leicester City na Januari
14, 2017 alicheza mechi yake ya Ligi Kuu England dhidi ya vinara wa ligi
hiyo Chelsea na timu yake ikashushiwa kipigo cha mabao 4-0.
Januari 2015 unamzungumzia Ndidi
anayecheza katika kikosi ambacho sasa tayari ni saizi ya Mtanzania
Mbwana Samatta. Mwaka mmoja baadaye, Ndidi ni mtu mwingine kabisa, yuko
katika kikosi cha Leicester, mabingwa wa England na kama utaweka vizuri
ni kwamba alikuwa anachuana na wachezaji kama akina Eden Hazard au siku
nyingine watu kama Zlatan Ibrahimovic au Mesut Ozil.
Sitaki kuzungumzia sana suala la umri
kwa kuwa Ndidi ana miaka 20 tu hadi sasa na Wanigeria au watu wa
Magharibi wamekuwa wakijaribu mara kwa mara kushusha. Lakini hoja ya
msingi ni mafanikio au hatua za kiungo huyo.
Kama Ndidi yuko Leicester kwani kipi
kitakachomzuia Samatta kufika hapo? Huenda nahodha huyo wa Taifa Stars
ambaye wote tunamjua ni mtu mwenye malengo na anayejituma kweli atakuwa
amepata changamoto kuu.
Maana ndani ya miezi minne, tayari
wachezaji wawili ambao anacheza nao mmoja amekwenda Bundesliga na
mwingine kapiga hatua hadi Premier League. Kama unakumbuka, Mjamaica
Leon Bailey amejiunga na Bayer Leverkusen ya Ujerumani. Huyu pia alikuwa
akicheza na Samatta katika ushambulizi na wakati mwingine waliunda
pacha bora kabisa.
Hizo ni kati ya ligi tatu bora za Ulaya
na duniani kote. Maana yake wana nafasi ya kusonga mbele zaidi na hii
inathibitisha jambo moja jingine kwamba Samatta hakukusea kwenda
Ubelgiji kwa kuwa ni njia sahihi.
Wengi wangependa kuona anakwenda nchi
kama Ufaransa na huo ndiyo ulikuwa mjadala wakati yeye anaondoka kwenda
nchini Ubelgiji baada ya kuiacha TP Mazembe.
Kwa hiyo hesabu zake zilikuwa sahihi na
alistahili kwenda kujiunga na timu ya Ubelgiji akiamini akifanya vema
ana nafasi ya kwenda katika moja ya ligi kubwa. Wako wanaotoka kutoka
alipo kwenda katika ligi hiyo.
Maana yake kwa yeye, mfano umfananishe
na Ndidi au Bailey, utaona Samatta amecheza michuano mikubwa kama ile ya
Kombe la Dunia akiwa na TP Mazembe, tena dhidi ya timu kubwa kama Inter
Milan na kadhalika.
Hivyo hali ya kujiamini na uwezo alionao haina shida wala shaka kwamba ana uwezo wa kufika huko walikofikia wenzake.
Lakini kitu kimoja, Bailey na Ndidi ni
kama wamempa ujumbe kwamba safari yake kwenda nje ya Ubelgiji haihitaji
kusubiri muda mrefu sana.
Badala yake juhudi za dhati kutaka kuondoka zinaweza kubadili mambo muda wowote na yeye akaanza safari hiyo mapema.
Ukweli ni hivi; Samatta yuko Ubelgiji
akiwa njiani kwenda Ufaransa, Italia, Ujerumani, Hispania au England na
lazima aende kama anataka kuwa kati ya wachezaji walioandika mafanikio
makubwa katika soka.
Hivyo hana sababu ya kusubiri sana kwa
sababu nyingi kwamba anahitaji kuzoea angalau misimu miwili, mitatu au
zaidi. Badala yake ni kuangalia njia sahihi ya kuondoka na kufikia
anapotaka.
Bailey na Ndidi ni kama wamefunga kamba
za viatu vyake na kumueleza kwamba asichoke na anaweza kuzifungua baada
ya kutua katika moja ya ligi hizo bora duniani. Mimi naamini inawezekana
na Samatta namuamini anaweza. Kila la kheri.
SOURCE: CHAMPIONI
0 Maoni:
Post a Comment