Na kiungo mshambuliaji twende wote;
MWAKA
2002, wakati Juma Kaseja anaanza kuichezea Simba akitokea Moro United,
Kipa Essam Kamal El Hadary tayari alikuwa kipa namba moja wa timu bora
kuliko zote Afrika ya Al Ahly.
El
Hadary alijiunga na Al Ahly mwaka 1996 baada ya kutamba na Damietta
aliyoichezea tangu 1993 hadi 1996.
Wakati
kipa Juma Kaseja wa Simba anaanza kuonekana “mzee” mwaka 2009, El
Hadary alikuwa anamalizana na FC Sion ya Uswisi ambayo alijiunga nayo
2008 na kuamua kurejea tena Misri kujiunga na Ismaily ambayo aliichezea
msimu mmoja halafu akajiunga na mahasimu wake hapo, kabla ya Zamalek
aliyocheza msimu mmoja hadi 2011 na kuondoka kwenda Al Merreikh ya
Sudan.
Kipindi
El Hadary anakwenda El Merreikh na kuwa mchezaji anayelipwa mshahara
mkubwa kuliko wote, ndiyo kipindi Wana-Simba “wataalamu umri”
walipohakikisha Kaseja anaondoka Simba kwa kuwa alikuwa amezeeka.
Kaseja
alikuwa hazina kwa Simba na taifa, alionekana hana uwezo tena, ni mzee.
Watu wakakubali kwa faida ya wachache ambao waliona umaarufu au ukubwa
wa Kaseja ni kama tatizo kwao. El Hadary akaendelea kucheza na kufanya
vema, juzi ameiongoza Misri kuingia kwenye fainali nyingine ya Kombe la
Mataifa Afrika (Afcon) na kama watawashinda Cameroon, basi litakuwa ni
kombe lake la tano, ameishatwaa katika miaka ya 1998, 2006, 2008 na
2010.
Usisahau
ametokea katika kizazi cha dhahabu cha Misri kilichoongozwa na akina
Mohamed Aboutrika. Leo anaendelea kucheza, pia ni kiongozi wa vijana
katika timu ya Misri.
Wakati
El Hadary anaichezea Misri kwa mara ya kwanza 1996, Ramadani Sobhi
ambaye anakipiga Stoke City ya England ndiyo alikuwa na umri wa mwaka
mmoja tu. Binti yake wa kwanza, ana umri sawa na huo wa Sobhi.
Sasa
El Hadary ameichezea timu ya Taifa ya Misri kwa zaidi ya miaka 20, sasa
anacheza na wajukuu zake na anaendelea kuwa tegemeo na gumzo.
Mechi
153 za kimataifa akiwa na Misri, pekee ni Gianluigi Buffon wa Italia,
Iker Casillas wa Hispania na Mohamed Al-Deayea wa Saudi Arabia ndiyo
makipa wanaoweza kufananishwa naye wakiwa wanamzidi kumfikia au kufanana
naye.
Watanzania
wakiwemo mashabiki na viongozi wa Simba, wanaweza kujifunza kupitia El
Hadary kwamba chuki ni tatizo, chuki inawaua wale ambao wangeweza kuwa
msaada.
Hakuna
ubishi, Kaseja bado alikuwa katika kiwango cha kuisaidia Simba zaidi.
Ndiyo maana unaona, tangu ameondoka hakuna kipa mzawa aliyefikia nusu ya
ubora wake na akawa msaada katika kikosi chao. Badala yake wamekuwa
wakihangaika na makipa wa kigeni ambao pia wanalazimika kuwabadili.
Maisha
ya Kaseja ndani ya Simba yalikuwa na thamani kubwa kwa kuwa alifanya
mengi kwa moyo wa dhati. Anachokifanya leo El Hadary ni funzo kuu kwa
vijana wa Misri na wengine wangependa kuvunja rekodi yake.
Kaseja
alivyoondoka Simba, inaonekana hakuna haja ya kujituma au kuitumikia
klabu muda mrefu kwa mafanikio kwa kuwa mwisho wake hauwezi kuwa na
heshima au manufaa.
Kaseja
kaondoka Simba kwa kuwa hata walio na mchezo usiofikia robo ya wa
kwake, waligeuka kuwa wenye nguvu na wakamng’oa. Leo anaendelea kufanya
kazi yake vizuri na huenda angekuwa bora zaidi kuliko sasa.
Kaseja
anaweza kuwa sehemu ya watoto wa El Hadary, lakini mazingira ya kazi
yake yalikuwa magumu kuliko El Hadary na akafanya vema zaidi. Hivyo
lazima Watanzania tujenge tabia ya kuheshimu michango ya wanaofanya vema
badala ya kuchukizwa na kuendelea kwao kufanya vema.
Haiwezekani
El Hadary akatamba kama miujiza tu. Lazima ndani yake kuna juhudi,
malengo na nidhamu ya juu bila ya kuyumba. Hali kadhalika, Kaseja
amekuwa hivyo. Watu wamemshusha kwa kumvika uzee. Yeye na El Hadary nani
mzee?
Lazima
tubadilike, la sivyo watu walio katika soka sasa watakuwa hawajui au
watashindwa kuelewa faida za kufanya vema kwa muda mrefu. Au watakosa
sababu ya kuona umuhimu wa kujituma kwa kuwa wana hofu na mwisho wao.
0 Maoni:
Post a Comment