Dar es Salaam. Wawakilishi wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga itaanzia nyumbani, Uwanja wa Taifa Dar es Salaam dhidi ya Zanaco ya Zambia mchezo wa kuwania kucheza hatua ya makundi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa timu zilizofuzu raundi ya awali, mchezo huo utapigwa kati ya Machi 11 na 13 na marudiano yatakuwa Lusaka, Zambia Machi 17 na 19.
Yanga imeingia hatua hiyo baada ya kuibandua N’gaya ya Comoro kwa mabao 6-2. Mchezo wa kwanza Yanga ilishinda 5-1 kabla ya kutoka sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam.
Zanaco iliipiga APR ya Rwanda bao 1-0 mjini Kigali wakati mchezo wa kwanza timu hiyo zilitoka suluhu mjini Lusaka.
Wakati Yanga ikianza nyumbani, wawakilishi wengine wa Kombe la Shirikisho, Azam, itacheza na Mbabane Swallows ya Swaziland Machi 12 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Afisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd alisema tayari Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Saady Kawemba ameiarifu CAF kuhusu tarehe na uwanja utakaotumika kwa mchezo huo.
“Kocha ameshapata ripoti ya mchezo uliopita kati ya Mbabane na Opara United na ameshanza kuzifanyia kazi tangu jana, haitakuwa mechi rahisi na mwalimu atautumia mchezo wa Ligi dhidi ya Stand na FA dhidi ya Mtibwa kupanga kufanya maandalizi,” alisema Jaffar.
Kocha Mkuu wa Azam, Aristico Cioaba amesema ana imani kikosi chake kitafunga mabao ya kutosha ili kuiwezesha timu yake kufika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Juzi, Azam iliichapa Mwadui ya Shinyanga mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi huku ikionyesha uwezo mkubwa katika kupanga mashambulizi.
Akizungumza na blog hii, Cioaba alisema tangu aanze jukumu la kuinoa timu hiyo amekuwa akiwasisitiza wachezaji wake kucheza kwa kasi hususani wanapokaribia goli la wapinzani.
“Nilianza na mshambuliaji mmoja Yahya (Mohammed) lakini nilikuwa na winga wawili Singano (Ramadhan) na Mahundi (Joseph).
Pia, timu yangu iliwakosa washambuliaji wengine ambao wana majeraha lakini nashukuru tumepata ushindi ambao ni wa kwanza kwangu. “Sipendi timu icheze taratibu inapokwenda langoni kwa wapinzani, tunatakiwa kuwa ‘aggressive’.
Wakati mwingine kutokana na aina ya mchezo ni vigumu kupata nafasi mbili au tatu za kufunga,” alisema kocha huyo wa zamani wa Adouana Stars ya Ghana.
0 Maoni:
Post a Comment