TANGU
wafungwe 4-0 na Chelsea huko Stamford Bridge hapo Oktoba 23, Manchester
United imekuwa Timu pekee ‘Isiyofungika’ kwenye EPL, Ligi Kuu England,
ikimaliza zaidi ya Miezi 5 bila kufungwa zikiwa ni mbio za Mechi 18.
Licha
kusakamwa na Mechi kedekede wakiwa Timu pekee wenye Mechi nyingi kupita
yeyote huko England, Jose Mourinho ameongoza Kikosi hicho kwa ufanisi
mkubwa na kuwawezesha Mwezi Februari kutwaa Taji kubwa walipobeba Kombe
la Ligi, EFL CUP.
Mwezi
Aprili wanakabiliwa na Mechi 9 na ingawa Mourinho amelalamikia ugumu wa
Ratiba yao lakini hilo ni dalili tosha ya mafanikio yao Msimu huu wao
wa kwanza chini ya Jose Mourinho ambao walikuwemo kwenye mbio za
Mashindano Manne na kutolewa tu Wiki 2 zilizopita kwenye FA CUP.
Hilo
limempa Mourinho nafasi ya kubadili Kikosi chake katika kila Mashindano
na kumwezesha kupata Kikosi imara cha kucheza EPL bila kufungwa.
Mtizame
Mchezaji wa Kimataifa wa Armenia, Henrikh Mkhitaryan, ambae kwenye
Mechi yake ya kwanza tu Klabuni hapo, walipofungwa na Man City Mwezi
Septemba, alitolewa nje lakini hilo halikumkatisha tamaa kwani aliibukia
kwenye UEFA EUROPA LIGI na kung’ara na kurudi tena Kikosi cha Kwanza.
Kushiriki
Mashindano mengi kumemfanya Mourinho azungushe Wachezaji kwenye kila
Mechi ya EUROPA LIGI, EFL CUP na FA CUP lakini kwenye Ligi panga pangua
wapo David de Gea; Antonio Valencia, Phil Jones, Marcos Rojo, Matteo
Damian; Ander Herrera, Michael Carrick; Henrikh Mkhitaryan/Juan Mata, Paul Pogba, Marcus Rashford; Zlatan Ibrahimovic.
Wafuatiliaji
wa hizo Mechi zao 18 ambazo hawakufungwa kwenye Ligi wamebaini Man
United hufungwa Goli chache, 11 tu, lakini pia kufunga chache, Bao 29
tu.
Hiyo ndiyo sababu kubwa Man United wako Nafasi ya 5 kwenye Ligi wakiwa Pointi 17 nyuma ya Vinara Chelsea.
Kwa
ujumla Man United wamefunga Bao 42 katika Mechi 27 za Ligi tofauti na
wenzao kama Liverpool waliofunga 62, Chelsea 59, Tottenham Hotspur 55,
City 54, Arsenal 56 na Everton 51.
Kitu
muhimu kwa Kikosi cha Mourinho kutofungwa Mechi 18 za Ligi ni Difensi
yake hasa ule upacha wa Sentahafu ya Marcos Rojo na Phil Jones huku
Ander Herrera akiwa nguzo kubwa kwenye Kiungo.
Walipofungwa
Mechi yao ya mwisho ya Ligi na Chelsea, upacha wa Sentahafu ulikuwa ni
wa Eric Bailly na Chris Smalling na kuumia kwao kukatoa mwanya kwa
Rojo-Jones kucheza pamoja na wao ni kati ya Wachezaji 6 waliocheza Mechi
nyingi kwenye hizo 18 ambazo hawakufungwa wakifuatia Herrera,
Ibrahimovic, Pogba na Kipa De Gea anaeongoza.
Lakini
tatizo kubwa ni ufungaji ambao umebaki kwa Zlatan Ibrahimovic pekee
aliefunga Jumla ya Mabao 26 Msimu huu na 11 kati ya Mechi 16 za Ligi
zilizopita.
Sasa
Mwezi Aprili Man United wanakabiliwa na Mechi 9 wakianzia Jumamosi Old
Trafford kucheza na West Brom na kisha Jumanne Everton watatua Uwanja
huo huo wakati Jumamosi inayofuatia watakuwa safarini Stadium of Light
kuivaa Timu ya Mkiani Sunderland inayoongozwa na Meneja wa zamani wa Man
United David Moyes.
Mbio
hizi za kutofungwa za Mechi 18 za Ligi ndio bora kabisa kwenye Ligi Kuu
England tangu Machi 2013 pale Kikosi chini ya Sir Alex Ferguson
kilivyofanya hivyo.
MAN UNITED – Ratiba Aprili 2017:
@@Saa za Bongo
01 APR: Man United v West Bromwich Albion, EPL, Saa 1700
04 APR: Man United v Everton, EPL, 2200
09 APR: Sunderland v Man United, EPL, 1530
13 APR: Anderlecht v Man United, Europa Ligi Robo Fainali, 2205
16 APR: Man United v Chelsea, EPL, 1800
20 APR: Man United v Anderlecht, Europa Ligi Robo Fainali, 2205
23 APR: Burnley v Man United, EPL, 1615
27 APR: Man City v Man United, EPL, 2200
30 APR: Man United v Swansea City, EPL, 1400
0 Maoni:
Post a Comment