Ni mchezo wa ligi ya Vodacom ambao unatabiriwa kuwa
kikwazo kwa kikosi cha Simba ambacho kinaongoza ligi kwa tofauti ya
pointi MOJA kati yao na mabingwa watetezi Yanga baada ya mchezo wa Yanga wa jana.
Kikosi cha Simba leo kitakuwa kinarudi tena kibaruani kusaka pointi tatu
zitakazoendelea kuwaweka kileleni mwa msimamo wakati watakapo wakabili
Maafande wa Ruvu Shooting kutoka Mlandizi mkoani Pwani mchezo ambao umepangwa kupigwa uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Pamoja na mechi hiyo kupigwa uwanja wa Uhuru, lakini Simba itahesabika kama ipo ugenini kutokana na uwanja unaotumiwa na Ruvu
Shooting wa Mabatini uliopo Mlandizi, kutokuwa na usalama wa kuhimili
uwingi wa mashabiki watakaoingia kwenye mechi za Simba au Yanga.
Ruvu wanaingia kwenye mchezo huo wakijivunia ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Tanzania Prisons wakati wageni wao Simba nao walipata ushindi wa tabu wa bao 1-0, wakiwa nyumbani uwanja wa Uhuru dhidi ya Ndugu zao JKT Ruvu.
Maafande hao watataka kushinda mchezo huo ili kuendelea kujiweka sawa
kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati Simba watahitaji ushindi ili kuzidi
kujikita kileleni mwa msimamo wakifikisha pointi 44.
Kocha wa Ruvu Shooting, Malale
Hamsini anajua vizuri mziki wa Simba hivyo leo atakuwa na kazi moja
ya kuwapunguza kasi Simba wasiendelee kupata matokeo ya ushindi leo.
Malale amesema anaijua Simba pamoja na mbinu zao wanazotumia na yeye atawapanga vizuri vijana wake kuhakikisha wanapata ushindi.
Kocha huyo aliyeifundisha JKT Ruvu mzunguko wa kwanza atakuwa
akimtegemea zaidi kiungo Jabir Aziz 'Stima' na mshambuliaji Kisiga ambao wote waliwahi kuichezea Simba siku za nyuma.
Kipa Said Kipao anatarajiwa kukaa langoni na kuwasumbua washambuliaji
wa Simba ambao bila shaka wataongozwa na Pastory Athanas ,
aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo akitokea Stand United.
Kwa upande wao Simba maandalizi yao yamekamilika na wana uhakika wa
kuendeleza wimbi lao la ushindi kama ilivyokuwa kwenye mechi mbili
zilizopita.
Kocha Omog, amesema kikosi chake cha leo hakitakuwa na mabadiliko
makubwa na kile kilichoanza kwenye mchezo wa JKT Ruvu, na kusisitiza
kuwa watacheza kwa umakini mkubwa ili kupata ushindi.
“Hatuwezi kuwadharau Ruvu, kwasababu ni timu nzuri ingawa mchezo wa
kwanza tuliwafunga mabao 3-1, lakini timu yao imekuwa ikibadilika sana
na leo lazima tupambane ili kupata pointi tatu,”amesema Omog.
Kiungo Mohamed Ibrahim ‘MO’
anatarajiwa kuanza sambamba na Mghana James Kotei kwenye eneo la kiungo
huku kipa mpya Daniel Agyei, akikaa lango ni kwa mechi yake ya tatu
kwenye ligi ya Vodacom Tanzania bila kuruhusu bao kwenye nyavu zake.
Mshambuliaji Laudit Mavugo naye anatarajiwa kuanza kikosi cha kwanza
baada ya kumaliza dakika 90 za mchezo uliopita akiwa benchi huku Mzamiru
Yasini na Shizza Kichuya kwa pamoja wakiwa kwenye eneo ushambuliaji kuwasaidia Mavugo na Pastory.
Kocha Omog, kama kawaida yake amesema atatumia mfumo wa 4-3-3, ili
kujaza viungo wengi kwenye eneo la kati lengo likiwa kuwazuia wapinzani
wao wasiweze kuipenya ngome yao na kuleta madhara.
0 Maoni:
Post a Comment