Kinara wa Ligi Kuu Bara, Simba inaondoka leo kwenda Zanzibar kushiriki Kombe la Mapinduzi ambalo limeanza jana, timu hiyo imetamba kuendeleza wimbi lake la ushindi kama ilivyo katika Ligi Kuu Bara.
Katika ligi kuu, Simba inaongoza ikiwa na pointi 44 ikifuatiwa na Yanga yenye 40 huku Azam FC ikiwa ya tatu na pointi 30.
Simba
ipo Kundi A na timu za Taifa Jang’ombe, URA, KVZ, Jang’ombe Boys,
inatarajiwa kucheza mechi yake ya kesho Jumapili dhidi ya Taifa
Jang’ombe saa 2:30 usiku kwenye Uwanja wa Amaan, wakitanguliwa na mechi
kati ya KVZ na URA saa 10:00 jioni uwanjani hapo.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, amesema: “Tunataka kuendeleza kasi yetu ya ushindi kwenye michuano hii ya Mapinduzi, hatutazubaa, tutaifunga kila timu.
“Pia tumepanga kuwatumia wachezaji ambao hatuwatumii sana kwenye ligi ili wapate nafasi ya kuboresha viwango vyao.”
Kati
ya wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza
cha Simba ni Laudit Mavugo, Frederick Blagnon, Hamad Juma, Peter Manyika
na Novalty Lufunga.
Mayanja alisema wamepanga kutengeneza mzunguko wa wachezaji katika michuano hiyo na watatoa kipaumbele kwa wachezaji wa benchi.
“Tulichokipanga
kama benchi la ufundi ni kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wetu wa
akiba ambao hawakutumika sana, tunataka kuona uwezo wao wa ndani ya
uwanja baada ya kukosa nafasi ya kucheza.
“Wachezaji
hao wa akiba tutawachanganya na wale wa kikosi cha kwanza tuliokuwa
tunawatumia kwenye ligi kuu na lengo letu ni kuwapumzisha nyota
waliotumika sana katika ligi kuu,” alisema Mayanja.
0 Maoni:
Post a Comment