MCHEZAJI
LEJENDARI wa Manchester United Rio Ferdinand amefunguka na kutoa undani
kuhusu Mechi ya Jumapili Uwanjani Old Trafford kati ya Man United na
Liverpool ikiwa ni Mechi ya EPL, Ligi Kuu England.
Hii ni Mechi ya Mahasimu wakubwa Kihistoria huko England, waliocheza Mechi yao ya kwanza kabisa Tarehe 28 Aprili 1894 wakati huo Manchester United ikiwa na Jina lake la mwanzo kabisa Newton Heath, Mechi ambayo ilibatizwa ‘Dabi ya Kaskazini-Magharibi’ ikizikutanisha Timu zinazotoka Miji Miwili tofauti, Manchester na Liverpool.
Rio, akiongea na Mtandao wa Man United, www.manutd.com, ameeleza: “Ukichukulia nini Manchester United na Liverpool wanaleta kwa pamoja kuhusu Historia, kumbukumbu na ushindi kwenye Ligi Kuu England na ile Ligi ya zamani, basi hamna Gemu yeyote inayofanana na Mechi kati yao. Mechi hii huleta nderemo nyingi na Wikiendi hii haitakuwa tofauti!”
Rio ameeleza zaidi: “Nadhani tunao Mameneja Bora Duniani hapa kwenye Ligi Kuu. Ukiwaondoa, pengine, Carlo Ancelotti, Diego Simeone na Zinedine Zidane, pengine tunao Bora hapa, wanaofurahisha na wenye hulka kubwa. Jose Mourinho ni mmoja wao na Jurgen Klopp pia ameleta msisimko mpya England!”
Kuhusu Klopp, Rio ametamka: “Jinsi anavyoisuka Timu yake Liverpool, inasisimua. Ni watamu kuwaangalia. Wanacheza kwa ari, wako moja kwa moja, wakishambulia kwa nguvu na wingi. Achilia mbali Klabu unayosapoti, Liverpool, chini ya Klopp, ni Timu nzuri kuitazama na hilo huwafanya wawe hatari. Wanashinda Gemu 3-2 au 4-3 na hio inaonyesha udhaifu wao kwenye Difensi lakini wakifunga zaidi ya Wapinzani wao basi watakuwa tishio kubwa!”
JE WAJUA HII?
Uso kwa Uso:
- Man United wameifunga Liverpool Mechi 79, Sare 53 na Kufungwa 65.
- Man United wametwaa Ubingwa wa England mara 20, mara ya mwisho ikiwa Mwaka 2013.
- Liverpool wametwaa Ubingwa wa England mara 18, mara ya mwisho ikiwa Mwaka 1990
Pia Rio ameeleza: “Matumaini makubwa kwa Jose Mourinho au United si kitu kigeni. Nadhani Jose amepata kazi ngumu mno kupita yeyote kati ya Timu kubwa ukiangalia Watu waliopo, kubadilisha fikra za Kikosi na hasa falsafa waliyopewa kwa Misimu kadhaa iliyopita na kulazimika kubadilisha kila kitu na hii ni kazi kubwa mno!”
Rio amefafanua: “Alichohitaji ni kugundua Fomesheni na Wachezaji wanaofiti humo. Amepata na humo yumo Michael Carrick. Nilizungumza wakati wa Louis van Gaal na David Moyes, Michael ni muhimu mno kwa Timu hii. Ni kitu cha wazi yeye ni mzuri mno akiwa na Mpira lakini ni muhimu mno kwa Difensi. Wale wanaotazama Soka kijuujuu wakitaka Soka la kuburudisha hawataona undani na uzuri wa Carrick katika ulinzi na kulinda Difensi yake ya Watu Wanne. Yeye ni miongoni mwa walio bora niliowahi kucheza nao! Nafikiri, kwa sasa, yeye ndio bora kupita yeyote!”
Ameendelea: “Wakinasa Mpira na Carrick akipokea Mpira, hatoi pasi ya upande, yeye atapenyeza mbele na kuvuka Viungo kufikia Mafowadi wake. Wachezaji wetu hatari ni Mafowadi na wanahitaji kupokea Mipira mapema. Kwa Miaka michache iliyopita tulikuwa tunacheza polepole na ilikuwa ngumu kuvunja ukuta wa Mtu 8 waliojipanga safu ya Mtu 4, Mtu 4. Hiyo ngumu kuwavunja lakini Carrick akicheza, akipata Mpira, yeye anapenyeza kuvuka ukuta huo na Mafowadi wetu wanapata nafasi za kupiga Mashuti. Magoli hufungwa hivyo. Yeye ni muhimu mno kwa sasa na kwa mbinu za Mourinho!”
“Kitu kingine muhimu kilichosaidia United kuwa bora zaidi ni kupanda kwa fomu za Wachezaji wao wapya Pogba, Mkhitaryan na Ibrahimovic. Hawa ni Mastaa wa Dunia. Na sasa tumerudi kusaini Mastaa wakubwa na si kama mwanzo. Akiwepo Mourinho, ni suala la muda tu na mambo yatakuwa safi. Kwa hili wimbi la sasa la mafanikio, kufuzu 4 Bora ni kitu kinachowezekana. Chochote zaidi ya hapo kitakuwa kitu kikubwa mno lakini kwangu kucheza UEFA CHAMPIONZ LIGI ndio lengo!”
Rio amesema zaidi: “Kwa haya, Mechi ya Wikiendi hii inakuwa kubwa zaidi kwa umuhimu wake. Siku zote Mechi hii ni kubwa lakini ukiangalia malengo ya Timu hizi, vipaji vya Wachezaji wao na ubora wa Mameneja wao, ni Gemu ambayo ni kubwa mno!”
0 Maoni:
Post a Comment