Kocha
Mkuu wa timu ya Mshikamano ya Dar es Salaam inayoshiriki Ligi Daraja la
Kwanza (FDL), Hamisi Kinonda amefunguka kuwa ilibaki kidogo wachezaji
wake wafie uwanjani katika mchezo wao wa juzi dhidi ya Lipuli ya Iringa
kutokana na kichapo kikali walichokumbana nacho.
Katika
mchezo huo wa Kundi A ambao Mshikamano ilikubali kichapo cha mabao 2-1
katika Uwanja wa Kichangani, Iringa,inadaiwa kuwa wachezaji wa
Mshikamano walipigwa na askari waliokuwa wakilinda amani uwanjani hapo
baada ya kumzonga mwamuzi.
Akizungumza
kocha huyo alisema chanzo cha wao kukumbana na kipigo hicho ni baada ya
mwamuzi wa pembeni kumshambulia mchezaji wao, Muhsin ambapo katika
kujihami ndipo wachezaji wake wakaanza kupigwa virungu na askari
waliokuwa uwanjani hapo.
“Yaani
tumekutana na wakati mgumu sana Iringa kwa tukio zima lilivyotutokea,
kule wenyewe wana msemo unasema kwamba mgeni lazima aache pointi tatu
kivyovyote vile na viongozi wote wanakuwa nyuma ya timu mwenyeji na
kuisapoti ili ipate kushinda.
“Sisi
ndiyo tulikuwa wa kwanza kupata bao na likadumu hadi kipindi cha kwanza
kinakwisha, wao wakaja kusawazisha. Zilipomalizika dakika tisini,
zikaongezwa sita.
“Dakika
ya mwisho kabisa mwamuzi akatoa maamuzi ya utata baada ya kuwapa
penalti wenyeji ambayo haikuwa halali maana ulikuwa mpira wa kona mabeki
wangu wakaokoa lakini refa akaweka penalti ambapo wachezaji wangu
wakahamaki na kuanza kumzonga.
“Lakini
ghafla akatokea mwamuzi wa pembeni ambaye akaenda kumpiga mchezaji
wangu kichwa, sasa katika hali ya yeye kujihami ndipo askari na watu wa
usalama waliokuwa uwanjani wakaanza kuwapiga kwa virungu wachezaji wangu
na timu nzima bila ya kuangalia sehemu gani ambayo wanapiga.
“Kutokana
na tukio hilo vijana wakataka kutoka uwanjani na kususia mechi lakini
kwa sababu hatukutaka kushushwa daraja kutokana na kugomea mchezo
nikawaamuru warudi uwanjani tumalizie mchezo.
“Niweke
wazi kwamba tumeumizwa na hali hiyo tuliyokutana nayo Iringa na sisi
kuepuka maafa zaidi baada ya mechi tu tulichukua gari na kurejea Dar
kwani tuliamini kama tukilala pale kungekuwa na hatari ya wenyeji wetu
kuja kutufanyia unyama zaidi ya ule wa uwanjani.
“Ukiacha
kupigwa virungu na pia wachezaji wa Lipuli walikuwa wanawapiga ngumi za
waziwazi wachezaji wangu na utaona kuna mmoja ambaye alivimba jicho
baada ya kupigwa huko lakini mwamuzi wala hakuchukua maamuzi yoyote
yale,” alisema Kinonda.
0 Maoni:
Post a Comment