METHOLD MWANJALI MWEZI MMOJA TUZO TATU.

Tokeo la picha la Methold Mwanjali image
Kama kuna mwezi ambao hautosahaulika kwa beki kisiki wa Simba Methold Mwanjali kwenye historia yake ya soka, basi ni mwezi Januari mwaka huu.

Beki huyo raia wa Zimbabwe, lakini wazazi wake wakiwa na asili ya Tanzania, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo tatu tofauti.

Beki huyo mtulivu, asiye na papara, anayetumia akili zaidi na nguvu pale inapobidi, huku ikiwa ni aghalabu sana kupata kadi, amepachikwa jina na wanachama na mashabiki wa Simba wakimwita ‘Baba Mwenye Nyumba.’

Amekuwa mhimili mkubwa kwenye safu ya ulinzi ya Simba ambayo haikuwa nzuri sana msimu uliopita, iliyokuwa ikiruhusu magoli kirahisi. Mpaka sasa Simba imefungwa magoli sita, ikiwa ni magoli machache zaidi kuliko timu yoyote ile kwenye Ligi Kuu.

Kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Simba ilifungwa magoli mawili tu, moja ikiwa ni siku ya fainali na lingine la kujifunga wenyewe dhidi ya Taifa Jang’ombe, ikishinda mabao 2-1.


1. Mchezaji bora Kombe la Mapinduzi.
Mwanjali alipata tuzo yake ya kwanza mwezi huu, alipochaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Mara baada ya michuano hiyo kwisha na Azam kutwaa kombe kwa kuifunga Simba bao 1-0, jopo la makocha waliokuwa wakifuatilia michuano hiyo walimchagua beki huyo kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo.

2. Mchezaji bora wa klabu ya Simba
Siku chache baadaye, klabu ya Simba ikamtangaza rasmi kuwa mchezaji wao bora kwa mwezi Desemba.
Klabu ya Simba ina utaratibu wake wa kuchagua mchezaji bora kila mwezi. Ilibuni utaratibu huo ili kufanya wachezaji wa timu hiyo kujituma uwanjani na kuipa klabu yao mafanikio.
Kwa mwezi Desemba, Mwanjale ndiye kinara wa wachezaji wote wa Simba aliyefanya vizuri, na klabu hiyo kama kawaida yake ilimtuza.

3. Mchezaji bora wa Ligi Kuu
Kama vile haitoshi,  wiki hii amechaguliwa tena kuwa mchezaji bora Desemba wa Ligi Kuu msimu wa 2016/2017.
Amewashinda kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima na beki Yakubu Mohamed wa Azam FC.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF),  mwezi Desemba zilichezwa raundi tatu za ligi, huku Simba ikicheza mechi mbili ugenini na moja nyumbani. Raundi hizo ni za 16, 17 na 18.


Beki huyo wa kati, aliiongoza Simba kushinda mechi zote tatu, hivyo timu yake kupata ushindi wa asilimia 100 kwa kunyakua pointi zote tisa, na kubaki katika nafasi yao ya kwanza kwenye msimamo wa ligi, nafasi ambayo walikuwa nayo wakati wanaingia raundi ya 16.


Pia katika raundi hizo tatu ambapo Simba haikufungwa bao hata moja, Mwanjali alicheza dakika zote 270, na bila kuonyeshwa kadi yoyote. Alichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya timu yake huku akiongoza safu ya ulinzi.
Kwa kushinda tuzo hiyo beki huyo anajinyakulia kiasi cha Sh. Milioni.moja kutoka kwa wadhamini, akiongezea vitita alivyopata kwenye tuzo mbili zilizopita.

Amewahi kuchezea mabingwa wa Afrika
Alizaliwa mwaka 1983 huko Hwange nchini Zimbabwe. Amezichezea timu mbalimbali zikiwemo Hwange FC, Shabanie Mine na CAPS United zote za nchini Zimbabwe.
Aliondoka na kwenda nchini Afrika Kusini ambako alicheza soka la kulipwa kwenye klabu za Afrika Kusini kati ya 2010 hadi 2015, kabla ya kujiunga na Simba msimu huu.
Timu hizo ni Mpumalanga Black Aces FC na Mamelodi Sundowns ambao kwa sasa ni mabingwa wa soka Afrika. Pia aliwahi kuichezea timu ya taifa ya Zimbabwe na kuwahi kuwa nahodha wa timu hiyo mwaka 2011.
Awali alipojiunga na Simba hakutarajiwa kama anaweza kuoneha kiwango kikubwa, kutokana na umri wake kuonekana mkubwa, lakini uwezo wake na umri ni vitu viwili tofauti.
Share on Google Plus

About KASSIM OMARY

HII NI BLOG AMBAYO ITAKUWA INAKUPA HABARI MOTOMOTO ZA KIMICHEZO NA HABARI KWA UJUMLA
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 Maoni:

Post a Comment