Fainali za 11 za michuano ya Kombe la Mapinduzi zinatarajiwa kupigwa leo kwenye dimba la Amaan Visiwani Zanzibar kwa kuzikutanisha timu za Simba na Azam zote za Dar es Salaam.
Azam ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kutinga hatua hiyo ya fainali kwa kuifunga Taifa Jang’ombe
bao 1-0, wakati Simba ilipambana na wapinzani wao wa jadi Yanga na
kushinda kwa penati 4-2, baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika
muda wa kawaida wa dakika 90.
Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na
timu hizo kufahamiana vizuri , kutokana na zote kushiriki ligi ya
Vodacom Tanzania Bara.
Simba inayotokea kundi A, katika michuano hiyo inapewa nafasi kubwa
ya kushinda mchezo huo kutokana na ubora ambao iliuonyesha katika mechi
zake zilizopita ingawa imekuwa na tatizo kubwa kwenye safu ya
ushambuliaji.
Kocha wa Simba Joseph Omog,
amepania kulitwaa taji hilo, kwa lengo la kuondoa ukame wa makombe
ambayo umeikumba klabu hiyo kwa misimu minne iliyopita pasipo kubeba
ubingwa wowote.
Ukimuondoa beki Juuko Murshind, wachezaji wengine wote wapo kwenye
kikosi cha Mcameroon, huyo ambaye ametua Simba msimu huu, baada ya
kutimuliwa na Azam misimu miwili iliyopita.
Omog anawajua vizuri wapinzani wake Azam na bila shaka kesho atapanga
kikosi imara kwa ajili ya kupata ushindi wa mapema, ili kutimiza adhima
yake ya kubeba taji hilo ambalo litakuwa la pili, baada ya mara ya
kwanza kuchukua ikiwa na Azam FC.
Kikosi cha Simba hakitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa na kile
kilichoanza mchezo uliopita, dhidi ya Yanga na watakuwa wanamtegemea
zaidi kipa wao Daniel Angyei, ambaye alidaka penati mbili na kuivusha
timu hiyo fainali.
Beki Abdi Banda na Method Mwanjali wanatarajia kuanza kwenye ulinzi
wa kati huku Mohamed Hussein na Jamvier Bukungu mfungaji wa penati ya
mwisho naye akitarajiwa kuanza kwenye beki wa kuli.
Mshambuliaji Ibrahim Ajibu leo anatarajiwa kucheza mechi yake ya
kwanza kwenye mashindano hayo, akianza sambamba na Juma Luizio, ambaye
ameonekana akiwa na mchango mkubwa tangu alipoanza kupewa nafasi na
kocha Omog, huku wakisaidiwa na Mohamed Ibrahim ‘MO’ na James Kotei
kwenye eneo la kiungo.
“Mfumo ambao nitatumia kwenye mchezo wa leo ni 4-3-3 nimeamua
kufanya hivyo ili kuwa na watu wengi katikati kwasababu madhara ya Azam
yapo kwenye eneo la kiungo kama unawaacha kutawala unaweza kupata tabu
na ndicho kilichowakuta Yanga kwenye mchezo ambao walishinda
4-0,”amesema Omog.
Kwaupande wao Azam kocha wake Idd Cheche, ametamba kuifunga Simba kwa
kutumia mbinu zile alizozitumia kwa Yanga, kubeba kombe hilo ikiwa ni muda mfupi tangu kupewa timu.
Cheche amesema anatambua kuwa ni mchezo mgumu, lakini wamejipanga
vizuri kuhakikisha wanamaliza vizuri michuano hiyo baada ya kuanza
vibaya kwa kucheza kiwango kisichoridhisha.
Kocha huyo amesema anaimani kubwa na wachezaji wake kutokana na
maelekezo ambayo amewapa na endapo watayafatisha kama alivyowaelekeza
anauhakika wa ushindi baada ya dakika 90 za mchezo huo alioupa umuhimu
mkubwa kabisa.
Cheche amesema kikosi chake cha leo hakitabadilika kwani,
ukilinganisha na kile kilichoanza katika mchezo uliopita dhidi ya Taifa
Jang’ombe.
Aishi Manula anatarajiwa kuanza langoni sambamba na Aggrey Moris na
Yakub Mohamed raia wa Ghana na katika safu ya ushambuliaji kocha Cheche
itaendelea kuwategemea washambuliaji wake wawili Yahya Mohamed na
nahodha wake John Bocco ambaye alifunga bao la kwanza kwenye mchezo
dhidi ya Yanga.
Abubakar Salum Sure Boy, anatarajia kuwepo kwenye eneo la kiungo
akisaidiana na Frank Domayo mfungaji wa bao lililoivusha timu hiyo
kwenye fainali dhidi ya Jang’ombe Jumanne iliyopita.
Vita kubwa katika mchezo huo inatarajiwa kuwa katika eneo la kiungo
ambapo James Kotei wa Simba atakapo pambana vikali na Sure Boy na Domayo
ambao wameonekana kuwa nguzo muhimu kwa Azam.
Kipa wa Simba anatarajiwa kufanya kazi ya zaida zaidi ya ilivyokuwa
kwenye mchezo dhidi ya Yanga kwasababu Azam imeonyesha kuwa na makali
kwenye safu yake ya ushambuliaji kwa kuwatumia Bocco na Mohamed.
Wakati kipa wa Simba akitarajiwa kuwa na wakati mgumu Aishi Manula wa
Azam yeye anatarajiwa kuwa likizo kwa muda mrefu kutokana na ubutu wa
safu ya ushambuliaji wa Simba ambao umekuwa hautishi kama ilivyokuwa
timu nyingine kwenye mashindano hayo.
0 Maoni:
Post a Comment