Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea rufaa kutoka
Klabu ya Polisi Dar es Salaam dhidi ya Klabu ya Simba kuhusu
kumchezesha Mchezaji Novalty Lufunga katika mchezo wao wa Raundi ya Tano
ya Kombe la Azam Sports Federation Cup 2017.
Madai ya Polisi ni kwamba Mchezaji Novalty Lufunga alioneshwa kadi
nyekundu kwenye mchezo kati ya Simba na Coastal Union katika mchezo wa
Azam Sports Federation Cup 2015/2016 uliofanyika Uwanja wa Taifa, Aprili
11, mwaka jana.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetupilia mbali rufaa
hiyo kwa kukosa vigezo vya kikanuni katika uwasilishaji wake na hivyo
kukosa sifa ya kusikilizwa. Hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) na (2)
ya Kanuni za Kombe la Shirikisho la Azam Sports HD.
Kanuni ya 18 (1) inasema: “Malalamiko yoyote kuhusiana na mchezo
yawasilishwe kwa maandishi kwa kamishna wa mchezo au TFF sio zaidi ya
masaa sabini na mbili (72hrs) baada ya kumalizika mchezo.”
Kanuni ya 18 (2) inasema: Ada ya malalamiko ni shilingi laki tatu
(Tshs 300,000.00). Malalamiko yo yote yatakayowasilishwa bila kulipiwa
ada na kuwasilishwa nje ya muda uliowekwa hayatasikilizwa.”
Hata hivyo, Shirikisho linapenda kutoa ufafanuzi kuhusu kadi
nyekundu aliyopewa Mchezaji Novalty Lufunga katika mashindano ya Azam
Sports Federation Cup 2016/2017.
Kwa utaratibu wa mashindano haya ambayo ni ya mtoano, adhabu za
kadi (njano na nyekundu) zitolewazo uwanjani, zinakoma mwisho wa msimu
wa shindano husika isipokuwa kadi hizo zikiongezwa adhabu ya kinidhamu
(suspension) ambayo itafahamisha kwa klabu na mchezaji kwa maandishi.
Kadhalika, Kanuni ya 16 ya Kanuni za Kombe la Shirikisho Sehemu ya
Tatu inaeleza wazi kuwa matumizi ya kanuni za ligi zitahusika maeneo
yanayoruhusu uendeshaji wa shindano la mtoano.
“Adhabu zote zinazohusisha katika mashindano ya Kombe la Shirikisho
la Azam HD zitahusisha na shindano hili tu,” inasema kanuni ya 16 (3)
na (4).
KAMBI YA KILIMANJARO WARRIORS
Timu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23
‘Kilimanjaro Warriors’ inatarajiwa kuingia kambini Janauri 29, 2017 kwa
ajili ya maandalizi ya awali ya kucheza mechi za kufuzu fainali za
Olimipiki zitakazofanyika jijini Tokyo, Japan mwaka 2020.
Kambi hiyo ya wiki moja itafanyika kwenye Hosteli za Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambako pia kuna Uwanja wa Karume, Ilala
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mazoezi kulingana na program za
walimu.
Tanzania haijapata kushiriki Michuano ya Olimpiki kwa upande wa
mpira wa miguu jambo ambalo limeisukuma TFF kuona kuwa ni fursa ya mpira
wa miguu kuchezwa hivyo inashirikiana na Kamati ya Olimpiki Tanzania
(TOC), kufanikisha mipango na taratibu.
Tanzania kwa sasa ina vijana wengi waliotokana na michuano ya Mradi
wa kuibua na kukuza vipaji wa Airtel kadhalika na Cocacola ambao
wamekuwa chachu ya maendeleo ya timu ya taifa ya vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys.
Vijana hawa wa Airtel, Copa Cocacola na Serengeti Boys wataungana
na baadhi ya vijana waliofanya vizuri kwenye Ligi ya Vijana wenye umri
wa chini miaka 20 kutoka timu za Ligi Kuu ambao wamezaliwa baada ya
tarehe 1 Januari 1997 ili kuunda kikosi imara cha awali kuelekea kufuzu
kwa michuano ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo Japan, mwaka 2020.
Kwa kufuata utaratibu wa maandalizi ya Serengeti Boys na kwa
kushirikiana na TOC timu hii itapewa mazoezi na michezo ya kujipima
nguvu ndani na nje ya nchi.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
0 Maoni:
Post a Comment